Zaburi 125
Usalama wa watu wa Mwenyezi Mungu
Wimbo wa kwenda juu.
Wale wamtumainio Mwenyezi Mungu ni kama Mlima Sayuni,
ambao hauwezi kutikisika, bali wadumu milele.
Kama milima inavyozunguka Yerusalemu,
ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowazunguka watu wake
sasa na hata milele.
 
Fimbo ya waovu haitadumu juu ya nchi
waliyopewa wenye haki,
ili wenye haki wasije wakatumia
mikono yao kutenda ubaya.
 
Ee Mwenyezi Mungu, watendee mema walio wema,
wale walio wanyofu wa moyo.
Bali wale wanaogeukia njia zilizopotoka,
Mwenyezi Mungu atawafukuza pamoja na watenda maovu.
 
Amani iwe juu ya Israeli.