Zaburi 126
Kurejeshwa kutoka uhamisho
Wimbo wa kwenda juu.
Mwenyezi Mungu alipowarejesha mateka Sayuni,
tulikuwa kama watu walioota ndoto.
Vinywa vyetu vilijaa kicheko,
ndimi zetu zilijaa nyimbo za shangwe.
Ndipo iliposemwa miongoni mwa mataifa,
“Mwenyezi Mungu amewatendea mambo makuu.”
Mwenyezi Mungu ametutendea mambo makuu,
nasi tumejaa furaha.
 
Ee Mwenyezi Mungu, turejeshee watu wetu waliotekwa,
kama vijito katika Negebu.
Wapandao kwa machozi
watavuna kwa nyimbo za shangwe.
Yeye azichukuaye mbegu zake
kwenda kupanda, huku akilia,
atarudi kwa nyimbo za shangwe,
akichukua miganda ya mavuno yake.