Zaburi 127
Bila Mwenyezi Mungu, kazi ya mwanadamu haifai
Wimbo wa kwenda juu. Wa Sulemani.
Mwenyezi Mungu asipoijenga nyumba,
wajengao hufanya kazi bure.
Mwenyezi Mungu asipoulinda mji,
walinzi wakesha bure.
Mnajisumbua bure kuamka mapema
na kuchelewa kulala,
mkitaabikia chakula:
kwa maana yeye huwapa usingizi wapendwa wake.
 
Watoto ni urithi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu,
uzao ni zawadi kutoka kwake.
Kama mishale mikononi mwa shujaa
ndivyo walivyo wana awazaao mtu katika ujana wake.
Heri mtu ambaye podo lake
limejazwa nao.
Hawataaibishwa wanaposhindana
na adui zao langoni.