Zaburi 128
Thawabu ya kumtii Mwenyezi Mungu
Wimbo wa kwenda juu.
Heri wale wote wamchao Mwenyezi Mungu,
wanaoenda katika njia zake.
Utakula matunda ya kazi yako;
baraka na mafanikio vitakuwa vyako.
Mke wako atakuwa kama mzabibu uzaao
ndani ya nyumba yako;
wana wako watakuwa kama machipukizi ya mizeituni
kuizunguka meza yako.
Hivyo ndivyo atakavyobarikiwa
mtu amchaye Mwenyezi Mungu.
 
Mwenyezi Mungu na akubariki kutoka Sayuni
siku zote za maisha yako,
na uone mafanikio ya Yerusalemu,
nawe ujaliwe kuishi uone watoto wa watoto wako.
 
Amani iwe juu ya Israeli.