Zaburi 129
Maombi dhidi ya adui za Israeli
Wimbo wa kwenda juu.
Wamenitesa sana tangu ujana wangu;
Israeli na aseme sasa:
wamenitesa sana tangu ujana wangu,
lakini bado hawajanishinda.
Wakulima wamelima mgongo wangu,
na kufanya mifereji yao mirefu.
Lakini Mwenyezi Mungu ni mwenye haki;
amenifungua toka kamba za waovu.
 
Wale wote wanaoichukia Sayuni
na warudishwe nyuma kwa aibu.
Wawe kama majani juu ya paa,
ambayo hunyauka kabla hayajakua;
kwa hayo mvunaji hawezi kujaza vitanga vyake,
wala akusanyaye kujaza mikono yake.
Wale wapitao karibu na wasiseme,
“Baraka ya Mwenyezi Mungu iwe juu yako;
tunakubariki katika jina la Mwenyezi Mungu.”