Zaburi 130
Kumngojea Mwenyezi Mungu
Wimbo wa kwenda juu.
Kutoka vilindini ninakulilia, Ee Mwenyezi Mungu.
Ee Bwana, sikia sauti yangu.
Masikio yako na yawe masikivu
kwa kilio changu unihurumie.
 
Kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu, ungeweka kumbukumbu ya dhambi,
Ee Bwana, ni nani angeweza kusimama?
Lakini kwako kuna msamaha,
kwa hiyo wewe unaogopwa.
 
Namngojea Mwenyezi Mungu, nafsi yangu inangojea,
katika neno lake naweka tumaini langu.
Nafsi yangu inamngojea Bwana
kuliko walinzi waingojeavyo asubuhi,
naam, kuliko walinzi
waingojeavyo asubuhi.
 
Ee Israeli, mtumaini Mwenyezi Mungu,
maana kwa Mwenyezi Mungu kuna upendo usiokoma,
na kwake kuna ukombozi kamili.
Yeye mwenyewe ataikomboa Israeli
kutoka dhambi zao zote.