Zaburi 133
Sifa za pendo la undugu
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
1 Tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza
ndugu wanapoishi pamoja katika umoja!
2 Ni kama mafuta ya thamani yaliyomiminwa kichwani,
yakitiririka kwenye ndevu,
yakitiririka kwenye ndevu za Haruni,
hadi kwenye upindo wa mavazi yake.
3 Ni kama umande wa Hermoni
ukianguka juu ya Mlima Sayuni.
Kwa maana huko ndiko Mwenyezi Mungu alikoamuru baraka yake,
naam, uzima hata milele.