Zaburi 135
Wimbo wa sifa kwa Mwenyezi Mungu
Msifuni Mwenyezi Mungu.*kwa Kiebrania ni Hallelu Yah pia 135:3, 21.
 
Lisifuni jina la Mwenyezi Mungu,
msifuni, enyi watumishi wa Mwenyezi Mungu,
ninyi ambao mnatumika ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu,
katika nyua za nyumba ya Mungu wetu.
 
Msifuni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwema,
liimbieni sifa jina lake, kwa maana hilo lapendeza.
Kwa maana Mwenyezi Mungu amemchagua Yakobo kuwa wake mwenyewe,
Israeli kuwa hazina yake ya pekee.
 
Ninajua ya kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu,
kwamba Bwana wetu ni mkuu kuliko miungu yote.
Mwenyezi Mungu hufanya lolote apendalo,
mbinguni na duniani,
katika bahari na vilindi vyake vyote.
Hufanya mawingu kupanda kutoka miisho ya dunia;
hupeleka miali ya radi pamoja na mvua
na huleta upepo kutoka ghala zake.
 
Alimuua mzaliwa wa kwanza wa Misri,
mzaliwa wa kwanza wa wanadamu na wanyama.
Alipeleka ishara zake na maajabu katikati yako, ee Misri,
dhidi ya Farao na watumishi wake wote.
10 Aliyapiga mataifa mengi,
na akaua wafalme wenye nguvu:
11 Mfalme Sihoni na Waamori,
Ogu mfalme wa Bashani
na wafalme wote wa Kanaani:
12 akatoa nchi yao kuwa urithi,
urithi kwa watu wake Israeli.
 
13 Ee Mwenyezi Mungu, jina lako ladumu milele,
kumbukumbu za fahari zako,
Ee Mwenyezi Mungu, kwa vizazi vyote.
14 Maana Mwenyezi Mungu atawathibitisha watu wake,
na kuwahurumia watumishi wake.
 
15 Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu,
zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
16 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,
zina macho, lakini haziwezi kuona;
17 zina masikio, lakini haziwezi kusikia,
wala hakuna pumzi katika vinywa vyao.
18 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,
vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.
 
19 Ee nyumba ya Israeli, msifuni Mwenyezi Mungu;
ee nyumba ya Haruni, msifuni Mwenyezi Mungu;
20 ee nyumba ya Lawi, msifuni Mwenyezi Mungu;
ninyi mnaomcha, msifuni Mwenyezi Mungu.
21 Msifuni Mwenyezi Mungu kutoka Sayuni,
msifuni yeye aishiye Yerusalemu.
 
Msifuni Mwenyezi Mungu.

*Zaburi 135:1 kwa Kiebrania ni Hallelu Yah pia 135:3, 21.