Zaburi 137
Maombolezo ya Israeli uhamishoni 
  1 Kando ya mito ya Babeli tuliketi, tukaomboleza  
tulipokumbuka Sayuni.   
 2 Kwenye miti ya huko  
tulitundika vinubi vyetu,   
 3 kwa maana huko hao waliotuteka  
walitaka tuwaimbie nyimbo;  
watesi wetu walidai nyimbo za furaha;  
walisema, “Tuimbieni wimbo mmoja  
kati ya nyimbo za Sayuni!”   
 4 Tutaimbaje nyimbo za Mwenyezi Mungu,  
tukiwa nchi ya kigeni?   
 5 Nikikusahau wewe, ee Yerusalemu,  
basi mkono wangu wa kuume na usahau ujuzi wake.   
 6 Ulimi wangu ushikamane na kaakaa la kinywa changu  
kama sitakukumbuka wewe,  
kama nisipokufikiri Yerusalemu  
kuwa furaha yangu kubwa.   
 7 Kumbuka, Ee Mwenyezi Mungu, walichokifanya Waedomu,  
siku ile Yerusalemu ilipoanguka.  
Walisema, “Bomoa, bomoa  
hata misingi yake!”   
 8 Ee binti Babeli, uliyehukumiwa kuangamizwa,  
heri yeye atakayekulipiza wewe  
kwa yale uliyotutenda sisi:   
 9 yeye ambaye atawakamata watoto wako wachanga  
na kuwaponda juu ya miamba.