Zaburi 138
Maombi ya shukrani
Zaburi ya Daudi.
Nitakusifu wewe, Ee Mwenyezi Mungu, kwa moyo wangu wote,
mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako.
Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu,
nami nitalisifu jina lako
kwa ajili ya upendo wako
na uaminifu,
kwa maana umeitukuza ahadi yako
zaidi ya jina lako.
Nilipoita, ulinijibu;
ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari.
 
Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Mwenyezi Mungu,
wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako.
Wao na waimbe kuhusu njia za Mwenyezi Mungu,
kwa maana utukufu wa Mwenyezi Mungu ni mkuu.
 
Ingawa Mwenyezi Mungu yuko juu,
humwangalia mnyonge,
bali mwenye kiburi
yeye anamjua kutokea mbali.
Nijapopita katikati ya shida,
wewe unayahifadhi maisha yangu,
unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu,
kwa mkono wako wa kuume unaniokoa.
Mwenyezi Mungu atatimiza kusudi lake kwangu,
Ee Mwenyezi Mungu, upendo wako wadumu milele:
usiziache kazi za mikono yako.