9
Kuteuliwa kwa Israeli na Mwenyezi Mungu
1 Ninasema kweli katika Al-Masihi, wala sisemi uongo, dhamiri yangu inanishuhudia katika Roho wa Mungu. 2 Nina huzuni kuu na uchungu usiokoma moyoni mwangu. 3 Kwa maana ningetamani hata mimi nilaaniwe na kutengwa na Al-Masihi kwa ajili ya ndugu zangu hasa, wale walio wa kabila langu kwa jinsi ya mwili, 4 yaani watu wa Israeli. Hao ndio wenye kule kufanywa wana, ule utukufu wa Mungu, yale maagano, kule kupokea Torati, ibada ya kwenye Hekalu na zile ahadi. 5 Wao ni wa uzao wa baba zetu wa zamani, ambao kutoka kwao Al-Masihi alikuja kwa jinsi ya mwili kama mwanadamu, yeye ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote, mwenye kuhimidiwa milele! Amen.
6 Si kwamba neno la Mungu limeshindwa. Kwa maana si kila Mwisraeli ambaye ni wa uzao utokanao na Israeli ni Mwisraeli halisi. 7 Wala hawawi wazao wa Ibrahimu kwa sababu wao ni watoto wake, lakini: “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka.” 8 Hii ina maana kwamba, si watoto waliozaliwa kimwili walio watoto wa Mungu, bali ni watoto wa ahadi wanaohesabiwa kuwa uzao wa Ibrahimu. 9 Kwa maana ahadi yenyewe ilisema, “Nitakurudia tena wakati kama huu, naye Sara atapata mtoto wa kiume.”
10 Wala si hivyo tu, bali pia watoto aliowazaa Rebeka walikuwa na baba huyo huyo mmoja, yaani baba yetu Isaka. 11 Lakini, hata kabla hao mapacha hawajazaliwa au kufanya jambo lolote jema au baya, ili kusudi la Mungu la kuchagua lipate kusimama, 12 si kwa matendo, bali kwa yeye mwenye kuita, Rebeka aliambiwa, “Yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.” 13 Kama vile ilivyoandikwa, “Nimempenda Yakobo, lakini nimemchukia Esau.”
Mwenyezi Mungu hana upendeleo
14 Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha! 15 Kwa maana Mungu alimwambia Musa,
“Nitamrehemu yeye nimrehemuye,
na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”
16 Kwa hiyo haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutegemea huruma ya Mungu. 17 Kwa maana Maandiko yamwambia Farao, “Nilikuinua kwa kusudi hili hasa, ili nipate kuonesha uweza wangu juu yako, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani kote.”
18 Kwa hiyo basi, Mungu humhurumia yeye atakaye kumhurumia na humfanya mgumu yeye atakaye kumfanya mgumu.
19 Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?” 20 Lakini, ewe mwanadamu, u nani wewe ushindane na Mungu? “Je, kilichoumbwa chaweza kumwambia yeye aliyekiumba, ‘Kwa nini umeniumba hivi?’ ” 21 Je, mfinyanzi hana haki ya kufinyanga kutoka bonge moja vyombo vya udongo, vingine kwa matumizi ya heshima na vingine kwa matumizi ya kawaida?
22 Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu? 23 Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake? 24 Hivi vyombo ni sisi, ambao pia alituita, sio kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu wa Mataifa.
Yote yalitabiriwa katika Maandiko
25 Kama alivyosema Mungu katika Hosea:
“Nitawaita ‘watu wangu’
wale ambao si watu wangu;
nami nitamwita ‘mpendwa wangu’
yeye ambaye si mpendwa wangu,”
26 tena,
“Itakuwa hasa mahali pale walipoambiwa,
‘Ninyi si watu wangu,’
wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai.’ ”
27 Isaya anapaza sauti na kusema kuhusu Israeli kwamba:
“Ingawa idadi ya Waisraeli ni wengi kama mchanga wa pwani,
ni mabaki yao tu watakaookolewa.
28 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ataitekeleza
hukumu yake duniani kwa haraka
na kwa ukamilifu.”
29 Ni kama vile alivyotabiri Isaya, akisema:
“Kama Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni,
hakutuachia uzao,
tungekuwa kama Sodoma,
tungefanana na Gomora.”
Kutokuamini kwa Israeli
30 Kwa hiyo tuseme nini? Kwamba watu wa Mataifa ambao hawakutafuta haki, wamepata haki ile iliyo kupitia kwa imani. 31 Lakini Israeli, ambao walijitahidi kupata haki kupitia kwa sheria, hawakuipata. 32 Kwa nini? Kwa sababu hawakuitafuta kupitia kwa imani bali kupitia kwa matendo. Wakajikwaa kwenye lile “jiwe la kukwaza”. 33 Kama ilivyoandikwa:
“Tazama naweka katika Sayuni jiwe la kukwaza watu
na mwamba wa kuwaangusha.
Yeyote atakayemwamini
hataaibika kamwe.”