10
1 Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe. 2 Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wana juhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa. 3 Kwa kuwa hawakuijua haki ya Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu. 4 Kwa maana Al-Masihi ni ukomo wa sheria ili kila mtu aaminiye ahesabiwe haki.
Wokovu kwa watu wote
5 Musa anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” 6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Al-Masihi chini) 7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda Kuzimu*Kuzimu hapa kwa Kiyunani ni Abyss, yaani mahali pa wafu.?’ ” (yaani ili kumleta Al-Masihi kutoka kwa wafu). 8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu, ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Isa ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. 11 Kama Maandiko yanavyosema, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” 12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na mtu wa Mataifa, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Mwenyezi Mungu, ataokolewa.”
14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri Habari Njema!”
16 Lakini si wote waliotii Injili. Kwa maana Isaya asema, “Mwenyezi Mungu, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” 17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Al-Masihi. 18 Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana:
“Sauti yao imeenea duniani pote,
nayo maneno yao yameenea
hadi miisho ya ulimwengu.”
19 Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Musa asema,
“Nitawafanya mwe na wivu
kwa watu wale ambao si taifa.
Nitawakasirisha kwa taifa
lile lisilo na ufahamu.”
20 Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema,
“Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta.
Nilijifunua kwa watu
wale ambao hawakunitafuta.”
21 Lakini kuhusu Israeli anasema,
“Mchana kutwa nimewanyooshea
watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”