2
Ruthu akutana na Boazi
1 Basi Naomi alikuwa na jamaa wa upande wa mume wake, kutoka ukoo wa Elimeleki, mtu maarufu ambaye aliitwa Boazi.
2 Ruthu, Mmoabu, akamwambia Naomi, “Nitaenda mashambani nikaokote mabaki ya nafaka nyuma ya yule nitakayepata kibali machoni pake.”
Naomi akamwambia, “Nenda, binti yangu.” 3 Basi akaenda, akaokota mabaki ya nafaka mashambani nyuma ya wavunaji. Ikatokea kwamba alijikuta akifanya kazi kwenye shamba lililokuwa mali ya Boazi, ambaye alikuwa wa ukoo wa Elimeleki.
4 Papo hapo Boazi akarudi kutoka Bethlehemu, akawasalimu wavunaji, akasema, “Mwenyezi Mungu awe nanyi!”
Nao wakamjibu, “Mwenyezi Mungu akubariki.”
5 Boazi akamuuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule mwanamwali ni wa nani?”
6 Msimamizi akamjibu, “Ni yule Mmoabu aliyerudi kutoka nchi ya Moabu pamoja na Naomi. 7 Yeye aliomba, ‘Tafadhali niruhusu niokote na kukusanya miongoni mwa miganda nyuma ya wavunaji.’ Naye ameshinda shambani tangu asubuhi pasipo kupumzika, isipokuwa kwa muda mfupi kivulini.”
8 Kisha Boazi akamwambia Ruthu, “Binti yangu, nisikilize. Usiende kuokota mabaki ya mavuno katika shamba lingine, na usiondoke hapa. Kaa hapa na hawa wajakazi wangu. 9 Angalia shamba wanaume wanamovuna, ufuate nyuma yao. Nimewaamuru wanaume hawa wasikuguse. Wakati wowote ukiona kiu, nenda kwenye mitungi ukanywe maji waliyoyateka wanaume hawa.”
10 Aliposikia hili, akasujudu, uso wake ukagusa chini, akamwambia, “Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanijali mimi mgeni?”
11 Boazi akamjibu, “Nimeambiwa yote uliyomtendea mama mkwe wako tangu mume wako alipofariki, na jinsi ulivyomwacha baba yako na mama yako na nchi yako ulimozaliwa, ukaja kuishi na watu ambao hukuwafahamu awali. 12 Mwenyezi Mungu na akulipe kwa yale uliyoyatenda. Ubarikiwe kwa wingi na Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye umekimbilia mabawani mwake.”
13 Kisha Ruthu akasema, “Naomba niendelee kupata kibali machoni pako, bwana wangu. Kwa maana umenifariji na umezungumza kwa ukarimu na mjakazi wako, hata ingawa mimi si bora kama mmoja wa wajakazi wako.”
14 Wakati wa chakula, Boazi akamwambia Ruthu, “Karibia hapa. Kula mkate na uchovye ndani ya siki.”
Alipoketi pamoja na wavunaji, akampa nafaka zilizookwa. Akala kiasi alichotaka na kusaza. 15 Alipoinuka ili kuokota mabaki ya nafaka, Boazi akawaagiza watu wake, “Hata kama atakusanya kati ya miganda, msimzuie. 16 Badala yake, toeni masuke katika miganda, mwachieni ayaokote, na msimkemee.”
17 Basi Ruthu akaokota masazo shambani hata jioni. Akatwanga ile shayiri aliyokusanya, ikajaa efa moja*Efa moja ni sawa na kilo 22.. 18 Akaibeba na kuelekea mjini, naye mama mkwe wake akaona jinsi alivyoweza kuokota nafaka nyingi. Pia Ruthu akachukua kile alichobakiza baada ya kula na kushiba, akampa.
19 Basi mkwewe akamuuliza, “Je, umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Abarikiwe mtu yule aliyekujali.”
Ndipo Ruthu akamwambia mama mkwe wake kuhusu mtu ambaye alikuwa amemfanyia kazi katika shamba lake. Akasema, “Yule mtu niliyefanyia kazi kwake leo, anaitwa Boazi.”
20 Naye Naomi akamwambia mkwewe, “Mwenyezi Mungu ambariki! Hakuacha kuonesha fadhili zake kwa walio hai na kwa waliokufa.” Pia akamwambia, “Huyo mtu ni mmoja wa jamaa yetu wa karibu anayestahili kutukomboa.”
21 Kisha Ruthu, Mmoabu, akasema, “Hata aliniambia, ‘Kaa pamoja na watumishi wangu hadi watakapomaliza kuvuna nafaka yangu yote.’ ”
22 Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, “Binti yangu, itakuwa vyema wewe ufuatane na wajakazi wake, kwa sababu katika shamba la mtu mwingine wanaweza kukudhuru.”
23 Kwa hivyo Ruthu akafuatana na wajakazi wa Boazi, akaokota hadi mwisho wa mavuno ya shayiri na ya ngano. Naye aliishi na mama mkwe wake.