3
Ruthu na Boazi kwenye sakafu ya kupuria
Kisha Naomi akamwambia mkwewe, “Binti yangu, nitakutafutia pumziko ili upate mema. Je, Boazi, ambaye umekuwa pamoja na wajakazi wake, si ni jamaa yetu wa karibu? Usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri kwenye sakafu ya kupuria. Basi oga na ukajipake marashi, ujivalie nguo zako nzuri. Kisha uende kwenye sakafu ya kupuria, lakini angalia asijue kwamba upo pale hadi atakapomaliza kula na kunywa. Atakapoenda kulala, angalia mahali atakapolala. Kisha uende ufunue miguu yake, ulale. Naye atakuambia utakalofanya.”
Ruthu akajibu, “Lolote usemalo nitatenda.” Basi akashuka hadi kwenye sakafu ya kupuria, akafanya kila kitu mama mkwe wake alichomwambia kufanya.
Boazi alipomaliza kula na kunywa, naye akawa amejawa na furaha, alienda kulala mwisho wa lundo la nafaka. Ruthu akanyemelea polepole, akafunua miguu yake, na akalala. Usiku wa manane, kitu kilimshtua Boazi, akajigeuza, akagundua yupo mwanamke amelala miguuni pake.
Akauliza, “Wewe ni nani?”
Akajibu, “Ni mimi Ruthu, mjakazi wako. Uitande nguo yako juu yangu, kwa sababu wewe ndiwe jamaa wa karibu wa kutukomboa.”
10 Akamwambia, “Binti yangu, ubarikiwe na Mwenyezi Mungu. Wema huu wa sasa ni mkuu kushinda hata ule ulioonesha mwanzoni. Hukuwakimbilia vijana, wakiwa matajiri au maskini. 11 Sasa, binti yangu, usiogope. Nitakufanyia yote uliyoomba. Kwa maana mji wote wa watu wangu wanakujua kwamba wewe ni mwanamke mwenye tabia nzuri. 12 Ingawa ni kweli kwamba mimi ndiye jamaa aliye karibu, bado kuna mtu mwingine wa jamaa aliye karibu zaidi wa kukomboa kuliko mimi. 13 Wewe kaa hapa usiku huu, kisha asubuhi akikubali kukukomboa, vyema, na akomboe. La sivyo, kama hayuko tayari, hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo nitafanya hivyo. Lala hapa hadi asubuhi.”
14 Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake hadi asubuhi, akaondoka mapema pasipo mtu kuweza kumtambua mwenzake, maana Boazi alisema, “Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika kwenye sakafu ya kupuria.”
15 Pia akamwambia, “Leta shela yako uliyoivaa, uitandaze.” Naye alipoitandaza, akamimina vipimo sita vya shayiri, akamtwika. Kisha Ruthu akarudi zake mjini.
16 Basi Ruthu alipofika kwa mama mkwe wake Naomi, akamuuliza, “Je, binti yangu, ilikuwaje huko?”
Ndipo akamwelezea kila kitu Boazi alichomfanyia. 17 Akaendelea kusema, “Amenipa shayiri vipimo sita*Vipimo 6 vya shayiri ni sawa na kilo 15., akaniambia, ‘Usiende kwa mama mkwe wako mikono mitupu.’ ”
18 Kisha Naomi akasema, “Subiri binti yangu, hadi utakapojua kwamba hili jambo limeendaje. Kwa sababu mtu huyu hatatulia hadi akamilishe jambo hili leo.”

*3:17 Vipimo 6 vya shayiri ni sawa na kilo 15.