2
Mpendwa
1 Mimi ni ua la Sharoni,
yungiyungi ya bondeni.
Mpenzi
2 Kama yungiyungi kati ya miiba,
ndivyo alivyo mpendwa wangu kati ya wanawali.
Mpendwa
3 Kama mti wa mtofaa miongoni mwa miti ya msituni,
ndivyo alivyo mpenzi wangu
miongoni mwa wanaume vijana.
Ninafurahia kuketi kivulini mwa mwanaume huyu,
na tunda lake ni tamu kwangu.
4 Amenichukua hadi ukumbi wa karamu,
na bendera ya huyu mwanaume
juu yangu ni upendo.
5 Nitie nguvu kwa zabibu kavu,
niburudishe kwa matofaa,
kwa maana ninazimia kwa mapenzi.
6 Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu,
na mkono wake wa kuume unanikumbatia.
7 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza
kwa paa na kwa ayala wa shambani:
Msichochee wala kuamsha mapenzi
hata yatakapotaka yenyewe.
8 Sikiliza! Mpenzi wangu!
Tazama! Huyu hapa anakuja,
akirukaruka juu milimani
akizunguka juu ya vilima.
9 Mpenzi wangu ni kama paa au ayala mchanga.
Tazama! Anasimama nyuma ya ukuta wetu,
akitazama kupitia madirishani,
akichungulia kimiani.
10 Mpenzi wangu alizungumza na kuniambia,
“Inuka, mpendwa wangu,
mrembo wangu, tufuatane.
11 Tazama! Wakati wa masika umepita,
mvua imekwisha na ikapita.
12 Maua yanatokea juu ya nchi;
majira ya kuimba yamewadia,
sauti za njiwa zinasikika
katika nchi yetu.
13 Mtini unatunga matunda yake ya mwanzoni,
zabibu zinazochanua zaeneza harufu nzuri.
Inuka, njoo mpenzi wangu.
Mrembo wangu, tufuatane.”
Mpenzi
14 Hua wangu penye nyufa za majabali,
mafichoni pembezoni mwa mlima,
nioneshe uso wako,
na niisikie sauti yako,
kwa maana sauti yako ni tamu,
na uso wako unapendeza.
15 Tukamatie mbweha,
mbweha wale wadogo
wanaoharibu mashamba ya mizabibu,
mashamba yetu ya mizabibu yaliyochanua.
Mpendwa
16 Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake,
yeye hujilisha kati ya yungiyungi.
17 Hadi jua linapochomoza,
na vivuli vikimbie,
rudi, mpenzi wangu,
na uwe kama paa,
au kama ayala mchanga
juu ya vilima vya Betheri.