3
 1 Usiku kucha kwenye kitanda changu  
nilimtafuta yule moyo wangu umpendaye;  
nilimtafuta, lakini sikumpata.   
 2 Sasa nitaondoka na kuzunguka mjini,  
katika barabara zake na viwanja;  
nitamtafuta yule moyo wangu umpendaye.  
Kwa hiyo nilimtafuta lakini sikumpata.   
 3 Walinzi walinikuta  
walipokuwa wakizunguka mji.  
Nikawauliza, “Je, mmemwona  
yule moyo wangu umpendaye?”   
 4 Kitambo kidogo tu baada ya kuwapita  
nilimpata yule moyo wangu umpendaye.  
Nilimshika na sikumwachia aende  
hadi nilipomleta katika nyumba ya mama yangu,  
katika chumba cha yule aliyenichukua mimba.   
 5 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza  
kwa paa na kwa ayala wa shambani:  
Msichochee wala kuamsha mapenzi  
hata yatakapotaka yenyewe.   
 6 Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani  
kama nguzo ya moshi,  
anayenukia manemane na uvumba  
iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote  
vya mfanyabiashara?   
 7 Tazama! Ni gari la Sulemani  
likisindikizwa na mashujaa sitini,  
walio wakuu sana wa Israeli,   
 8 wote wamevaa panga,  
wote wazoefu katika vita,  
kila mmoja na upanga wake pajani,  
wamejiandaa kwa ajili ya vitisho vya usiku.   
 9 Mfalme Sulemani alijitengenezea gari;  
alilitengeneza kwa mbao kutoka Lebanoni.   
 10 Nguzo zake alizitengeneza kwa fedha,  
kitako chake kwa dhahabu.  
Kiti chake kilipambwa kwa zambarau,  
gari lake likanakshiwa njumu kwa upendo  
na binti za Yerusalemu.   
 11 Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni,  
mkamtazame Mfalme Sulemani akiwa amevaa taji,  
taji ambalo mama yake alimvika  
siku ya arusi yake,  
siku ambayo moyo wake ulishangilia.