5
Mpenzi  
 1 Nimekuja kwenye bustani yangu, dada yangu,  
bibi arusi wangu;  
nimekusanya manemane yangu pamoja  
na manukato yangu.  
Nimekula sega langu la asali na asali yangu;  
nimekunywa divai yangu na maziwa yangu.  
Rafiki  
Kuleni, enyi rafiki, mnywe;  
kunyweni ya kutosha, ee wapenzi.   
Mpendwa  
 2 Nililala lakini moyo wangu ulikuwa macho.  
Sikiliza! Mpenzi wangu anabisha:  
“Nifungulie, dada yangu, mpendwa wangu,  
hua wangu, usiye na hitilafu.  
Kichwa changu kimeloa umande,  
na nywele zangu manyunyu ya usiku.”   
 3 Nimevua joho langu:  
je, ni lazima nivae tena?  
Nimenawa miguu yangu:  
je, ni lazima niichafue tena?   
 4 Mpenzi wangu aliweka mkono wake kwenye tundu la komeo;  
moyo wangu ulianza kugonga kwa ajili yake.   
 5 Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu,  
mikono yangu ikidondosha manemane,  
vidole vyangu vikitiririka manemane,  
penye vipini vya komeo.   
 6 Nilimfungulia mpenzi wangu,  
lakini mpenzi wangu alishaondoka;  
alikuwa ameenda zake.  
Moyo wangu ulishuka kwa kuondoka kwake.  
Nilimtafuta lakini sikumpata.  
Nilimwita lakini hakunijibu.   
 7 Walinzi walinikuta  
walipokuwa wakifanya zamu za ulinzi mjini.  
Walinipiga, wakanijeruhi,  
wakaninyang’anya joho langu,  
hao walinzi wa kuta!   
 8 Enyi binti za Yerusalemu, ninawaagiza:  
mkimpata mpenzi wangu,  
mtamwambia nini?  
Mwambieni ninazimia kwa mapenzi.   
Rafiki  
 9 Je, mpenzi wako ni bora kuliko wengine namna gani,  
wewe uliye mzuri kupita wanawake wote?  
Je, mpenzi wako ni mzuri kuliko wengine, namna gani,  
hata unatuagiza hivyo?   
Mpendwa  
 10 Mpenzi wangu anang’aa, tena ni mwekundu,  
wa kuvutia miongoni mwa wanaume kumi elfu.   
 11 Kichwa chake ni dhahabu safi kuliko zote,  
nywele zake ni za mawimbi  
na ni nyeusi kama kunguru.   
 12 Macho yake ni kama ya hua  
kandokando ya vijito vya maji,  
aliyeogeshwa kwenye maziwa,  
yaliyopangwa kama vito vya thamani.   
 13 Mashavu yake ni kama matuta  
ya mimea ya manukato.  
Midomo yake ni kama yungiyungi  
inayodondosha manemane.   
 14 Mikono yake ni fimbo za dhahabu  
iliyopambwa kwa krisolitho.  
Mwili wake ni kama pembe ya ndovu iliyong’arishwa  
iliyopambwa na yakuti samawi.   
 15 Miguu yake ni nguzo za marumaru  
zilizosimikwa katika vitako vya dhahabu safi.  
Sura yake ni kama Lebanoni,  
bora kama miti yake ya mierezi.   
 16 Kinywa chake chenyewe ni utamu,  
kwa ujumla yeye ni wa kupendeza.  
Huyu ndiye mpenzi wangu, huyu ndiye rafiki yangu,  
ee binti za Yerusalemu.