6
Rafiki  
 1 Mpenzi wako ameenda wapi,  
ewe mzuri kupita wanawake wote?  
Mpenzi wako amegeukia njia ipi,  
tupate kumtafuta pamoja nawe?   
Mpendwa  
 2 Mpenzi wangu ameenda bustanini mwake,  
kwenye vitalu vya vikolezo,  
kujilisha bustanini  
na kukusanya yungiyungi.   
 3 Mimi ni wake mpenzi wangu,  
na mpenzi wangu ni wangu;  
yeye hujilisha kati ya yungiyungi.   
Mpenzi  
 4 Wewe ni mzuri, mpendwa wangu, kama Tirsa,  
unapendeza kama Yerusalemu,  
umetukuka kama jeshi lenye bendera.   
 5 Uyageuze macho yako mbali nami;  
yananigharikisha.  
Nywele zako ni kama kundi la mbuzi  
wanaoteremka kutoka Gileadi.   
 6 Meno yako ni kama kundi la kondoo  
wanaotoka kuogeshwa.  
Kila mmoja ana pacha lake,  
hakuna hata mmoja aliye peke yake.   
 7 Mashavu yako nyuma ya shela yako  
ni kama vipande viwili vya komamanga.   
 8 Panaweza kuwa na malkia sitini,  
masuria themanini,  
na mabikira wasiohesabika;   
 9 lakini hua wangu, mkamilifu wangu,  
ni wa namna ya pekee,  
binti pekee kwa mama yake,  
kipenzi cha yeye aliyemzaa.  
Wanawali walimwona na kumwita aliyebarikiwa;  
malkia na masuria walimsifu.   
Rafiki  
 10 Ni nani huyu atokeaye kama mapambazuko,  
mzuri kama mwezi, mwangavu kama jua,  
ametukuka kama nyota zinazofuatana?   
Mpenzi  
 11 Niliteremka kwenye bustani ya miti ya milozi  
ili kutazama machipuko ya bondeni,  
kuona kama mizabibu imechipua  
au kama mikomamanga imechanua maua.   
 12 Kabla sijang’amua,  
shauku yangu iliniweka  
katikati ya magari ya vita ya wakuu wangu.   
Rafiki  
 13 Rudi, rudi, ee Mshulami;  
rudi, rudi ili tupate kukutazama!  
Mpenzi  
Kwa nini kumtazama Mshulami,  
kama kutazama ngoma ya Mahanaimu*au majeshi mawili?