9
Hukumu juu ya adui za Israeli
1 Neno la unabii:
Neno la Mwenyezi Mungu liko kinyume na nchi ya Hadraki
na Dameski itakuwa mahali pa kupumzika,
kwa kuwa macho ya watu na ya makabila yote ya Israeli
yako kwa Mwenyezi Mungu;
2 pia juu ya Hamathi inayopakana nayo,
juu ya Tiro na Sidoni,
ingawa wana ujuzi mwingi sana.
3 Tiro amejijengea ngome imara,
amelundika fedha kama mavumbi,
na dhahabu kama taka za mitaani.
4 Lakini Bwana atamwondolea mali yake
na kuuangamiza uwezo wake wa baharini,
naye atateketezwa kwa moto.
5 Ashkeloni ataona hili na kuogopa;
Gaza atagaagaa kwa maumivu makali,
pia Ekroni, kwa sababu
matumaini yake yatanyauka.
Gaza atampoteza mfalme wake
na Ashkeloni ataachwa pweke.
6 Wageni watakalia mji wa Ashdodi,
nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti.
7 Nitaondoa damu vinywani mwao,
chakula kile walichokatazwa kati ya meno yao.
Mabaki yao yatakuwa mali ya Mungu wetu,
nao watakuwa viongozi katika Yuda,
naye Ekroni atakuwa kama Wayebusi.
8 Lakini nitailinda nyumba yangu
dhidi ya majeshi ya wanyang’anyi.
Kamwe mdhalimu hatashambulia watu wangu tena,
kwa maana sasa ninawachunga.
Kuja kwa Mfalme wa Sayuni
9 Shangilia sana, ee Binti Sayuni!
Piga kelele, Binti Yerusalemu!
Tazama, Mfalme wako anakuja kwako,
ni mwenye haki, naye ana wokovu,
ni mpole, naye amepanda punda,
mwana-punda, mtoto wa punda.
10 Nitaondoa magari ya vita kutoka Efraimu
na farasi wa vita kutoka Yerusalemu,
nao upinde wa vita utavunjwa.
Atatangaza amani kwa mataifa.
Utawala wake utaenea kutoka bahari hadi bahari,
na kutoka Mto*yaani Mto Frati hadi mwisho wa dunia.
11 Kwako wewe, kwa sababu ya damu ya agano langu nawe,
nitawaacha huru wafungwa wako
watoke kwenye shimo lisilo na maji.
12 Rudieni ngome yenu, enyi wafungwa wa tumaini;
hata sasa ninatangaza kwamba
nitawarejesheeni maradufu.
13 Nitampinda Yuda kama nipindavyo upinde wangu,
nitamfanya Efraimu mshale wangu.
Nitawainua wana wako, ee Sayuni,
dhidi ya wana wako, ee Uyunani,
na kukufanya kama upanga wa shujaa wa vita.
Mwenyezi Mungu atatokea
14 Kisha Mwenyezi Mungu atawatokea;
mshale wake utamulika kama radi.
Bwana Mungu Mwenyezi atapiga tarumbeta,
naye atatembea katika tufani za kusini,
15 na Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atawalinda.
Wataangamiza na kushinda
kwa mawe ya kutupa kwa kombeo.
Watakunywa na kunguruma kama waliolewa mvinyo;
watajaa kama bakuli linalotumika kunyunyizia
kwenye pembe za madhabahu.
16 Mwenyezi Mungu, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo
kama kundi la watu wake.
Watang’ara katika nchi yake
kama vito vya thamani kwenye taji.
17 Jinsi gani watavutia na kuwa wazuri!
Nafaka itawastawisha vijana wanaume,
nayo divai mpya vijana wanawake.