10
Mwenyezi Mungu ataitunza Yuda
Mwombeni Mwenyezi Mungu mvua wakati wa vuli;
ndiye Mwenyezi Mungu atengenezaye mawingu ya tufani.
Huwapa watu manyunyu ya mvua,
pia mimea ya shambani kwa ajili ya kila mtu.
Sanamu huzungumza udanganyifu,
waaguzi huona maono ya uongo;
husimulia ndoto ambazo si za kweli,
wanatoa faraja batili.
Kwa hiyo watu wanatangatanga kama kondoo
walioteseka kwa kukosa mchungaji.
 
“Hasira yangu inawaka dhidi ya wachungaji,
nami nitawaadhibu viongozi;
kwa kuwa Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni
atalichunga kundi lake,
nyumba ya Yuda,
naye atawafanya kama farasi
mwenye kiburi akiwa vitani.
Kutoka Yuda litatokea Jiwe la pembeni,
kutoka kwake vitatoka vigingi vya hema,
kutoka kwake utatoka upinde wa vita,
kutoka kwake atatoka kila mtawala.
Kwa pamoja watakuwa kama mashujaa
wanaokanyaga barabara za matope
wakati wa vita.
Kwa sababu Mwenyezi Mungu yu pamoja nao,
watapigana na kuwashinda wapanda farasi.
 
“Nitaiimarisha nyumba ya Yuda
na kuiokoa nyumba ya Yusufu.
Nitawarejesha kwa sababu
nina huruma juu yao.
Watakuwa kama watu ambao
sijawahi kuwakataa
kwa sababu mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao,
nami nitawajibu.
Waefraimu watakuwa kama mashujaa,
mioyo yao itafurahi kana kwamba ni kwa divai.
Watoto wao wataona na kufurahi,
mioyo yao itashangilia katika Mwenyezi Mungu.
Nitawaashiria na kuwakusanya ndani.
Hakika nitawakomboa,
nao watakuwa wengi
kama walivyokuwa mwanzoni.
Ijapokuwa niliwatawanya miongoni mwa mataifa,
hata hivyo wakiwa katika nchi za mbali
watanikumbuka mimi.
Wao na watoto wao watanusurika katika hatari
nao watarudi.
10 Nitawarudisha kutoka Misri
na kuwakusanya toka Ashuru.
Nitawaleta katika nchi ya Gileadi na Lebanoni,
na hapo hapatakuwa na nafasi ya kuwatosha.
11 Watapita katika bahari ya mateso;
bahari iliyochafuka itatulizwa
na vilindi vyote vya Mto Naili vitakauka.
Kiburi cha Ashuru kitashushwa,
nayo fimbo ya utawala ya Misri itatoweka.
12 Nitawaimarisha katika Mwenyezi Mungu,
na katika jina lake watatembea,”
asema Mwenyezi Mungu.