11
Fungua milango yako, ee Lebanoni,
ili moto uteketeze mierezi yako!
Piga yowe, ee msunobari,
kwa kuwa mwerezi umeanguka;
miti ya fahari imeharibiwa!
Piga yowe, enyi mialoni ya Bashani,
msitu mnene umefyekwa!
Sikiliza yowe la wachungaji;
malisho yao manono yameangamizwa!
Sikia ngurumo za simba;
kichaka kilichostawi sana
cha Yordani kimeharibiwa!
Wachungaji wawili
Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wangu: “Lilishe kundi lililokusudiwa kuchinjwa. Wanunuzi wake huwachinja na kuondoka pasipo kuadhibiwa. Wale wanaowauza husema, ‘Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, mimi ni tajiri!’ Wachungaji wao wenyewe hawawahurumii. Kwa kuwa sitawahurumia tena watu wa nchi,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitawakabidhi kila mtu mkononi mwa jirani yake na mfalme wake. Wataitenda jeuri nchi, nami sitawaokoa kutoka mikononi mwao.”
Kwa hiyo nikalilisha kundi lililotiwa alama kwa kuchinjwa, hasa kundi lililodhulumiwa sana. Kisha nikachukua fimbo mbili, moja nikaiita Fadhili na nyingine Umoja, nami nikalilisha kundi. Katika mwezi mmoja nikawaondoa wachungaji watatu.
Kundi la kondoo likanichukia, nami nikachoshwa nao, nikasema, “Sitakuwa mchungaji wenu. Waache wanaokufa wafe na wanaoangamia waangamie. Wale waliobakia kila mmoja na ale nyama ya mwenzake.”
10 Kisha nikachukua fimbo yangu inayoitwa Fadhili nikaivunja, kutangua agano nililofanya na mataifa yote. 11 Likatanguka siku hiyo; kwa hiyo wale waliodhulumiwa katika kundi, waliokuwa wakiniangalia wakajua kuwa hilo lilikuwa neno la Mwenyezi Mungu.
12 Nikawaambia, “Mkiona kuwa ni vyema, nipeni ujira wangu, la sivyo, basi msinipe.” Kwa hiyo wakanilipa vipande thelathini vya fedha.
13 Naye Mwenyezi Mungu akaniambia, “Mtupie mfinyanzi,” hiyo bei nzuri waliyonithaminia! Kwa hiyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha na kumtupia huyo mfinyanzi katika nyumba ya Mwenyezi Mungu.
14 Kisha nikaivunja fimbo yangu ya pili iitwayo Umoja, kuvunja undugu kati ya Yuda na Israeli!
15 Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Vitwae tena vifaa vya mchungaji mpumbavu. 16 Kwa maana ninaenda kumwinua mchungaji juu ya nchi ambaye hatamjali aliyepotea, wala kuwatafuta wale wachanga au kuwaponya waliojeruhiwa, wala kuwalisha wenye afya, lakini atakula nyama ya kondoo wanono na kuzirarua kwato zao.
17 “Ole wa mchungaji asiyefaa,
anayeliacha kundi!
Upanga na uupige mkono wake na jicho lake la kuume!
Mkono wake na unyauke kabisa,
jicho lake la kuume lipofuke kabisa!”