86
Maombi ya Daudi.
1 Sikia, Ee Yahwe, na unijibu, kwa kuwa ni maskini na mnyonge.
2 Unilinde, maana mimi ni mwaminifu; Mungu wangu, umuokoe mtumishi wako anayekuamini.
3 Unihurumie, Bwana, maana ninakulilia wewe mchana kutwa.
4 Umfurahishe mtumishi wako, maana ni kwako, Bwana, ninaomba.
5 Wewe, Bwana, ni mwema, na uko tayari kusamehe, na huonesha huruma kubwa kwa wale wanao kulilia wewe.
6 Yahwe, sikiliza maombi yangu; sikia sauti ya ombi langu.
7 Katika siku ya shida ninakuita wewe, kwa maana utanijibu.
8 Katikati ya miungu hakuna wa kufananishwa na wewe, Bwana. Hakuna matendo kama matendo yako.
9 Mataifa yote ambayo umeyafanya yatakuja kwako na kusujudu mbele zako, Bwana. nao wataliheshimu jina lako.
10 Kwa kuwa wewe ni mkuu na utendaye mambo ya ajabu; wewe pekee ndiwe Mungu.
11 Unifundishe njia zako, Yahwe. Kisha nitatembea katika kweli yako. Unifanye kukuheshimu wewe.
12 Bwana Mungu wangu, nitakusifu kwa moyo wangu wote; nitalitukuza jina lako milele.
13 Kwa maana uaminifu wa agano lako ni mkuu kwangu; wewe umeokoa uhai wangu kutoka chini kuzimuni.
14 Ee Mungu, wenye kiburi wameinuka dhidi yangu. Kundi la watu wenye vurugu wanautafuta uhai wangu. Nao hawakuheshimu wewe.
15 Lakini wewe, Bwana, ni mwenye huruma na neema, hukasiliki haraka, na mwingi katika uaminifu wa agano lako na kweli.
16 Unigeukie na unihurumie; mpe nguvu zako mtumishi wako; umuokoe mwana wa mjakazi wako.
17 Unioneshe ishara ya fadhila zako. Kisha wale wanichukiao wataziona na kuaibishwa kwa sababu yako; Yahwe, umenisaidia na kunifariji.