18
Mgawanyo wa nchi iliyobaki
1 Kusanyiko lote la Waisraeli wakakusanyika huko Shilo na kusimamisha Hema la Kukutania. Nchi ikawa chini ya utawala wao, 2 lakini palikuwa bado makabila saba ya Israeli ambayo yalikuwa hayajapokea urithi wao.
3 Hivyo Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtasubiri hata lini ili kuingia kumiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, amewapa? 4 Chagueni watu watatu kutoka kila kabila. Nitawatuma kukagua nchi hiyo na kuandika taarifa kuhusu mgawanyo wa urithi wa kila kabila. Kisha watarudi kwangu. 5 Mtaigawanya hiyo nchi katika sehemu saba. Yuda atabaki katika eneo lake upande wa kusini na nyumba ya Yusufu katika nchi yake upande wa kaskazini. 6 Baada ya kuandika maelezo ya hizo sehemu saba za nchi, yaleteni kwangu, nami nitawapigia kura mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. 7 Hata hivyo, Walawi hawatakuwa na sehemu miongoni mwenu, kwa maana huduma ya ukuhani kwa Mwenyezi Mungu ndio urithi wao. Nao Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase wameshapata urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, ambako Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliwapa.”
8 Watu hao walipokuwa wanaondoka kwenda kuikagua hiyo nchi, Yoshua akawaagiza, “Nendeni mkakague hiyo nchi na mwandike maelezo yake. Kisha mrudi kwangu, nami nitawapigia kura hapa Shilo mbele za Mwenyezi Mungu.” 9 Ndipo hao watu walipoondoka na kupita katika ile nchi. Wakaandika maelezo yake kwenye kitabu, mji kwa mji, katika sehemu saba na kurudisha taarifa kwa Yoshua huko kambini Shilo.
10 Basi Yoshua akawapigia kura huko Shilo mbele za Mwenyezi Mungu, na hapo akawagawia Waisraeli nchi kulingana na makabila yao.
Mgawo kwa Benyamini
11 Kura ya kwanza iliangukia kabila la Benyamini, kufuatana na koo zao. Eneo lao walilogawiwa lilikuwa kati ya kabila la Yuda na la Yusufu.
12 Upande wa kaskazini, mpaka wao ulianzia pale Yordani, kupitia kaskazini mwa mteremko wa Yeriko, na kuendelea magharibi kuingia katika nchi ya vilima, ukitokea kwenye jangwa la Beth-Aveni. 13 Kutoka hapo ulikatiza kwenye mteremko wa kusini mwa Luzu (yaani Betheli) na kushuka hadi Ataroth-Adari katika kilima kusini mwa Beth-Horoni ya Chini.
14 Kutoka kilima kinachotazamana na Beth-Horoni upande wa kusini mpaka ule ukazunguka kusini kufuatia upande wa magharibi, na ukatokezea Kiriath-Baali (yaani Kiriath-Yearimu), mji wa watu wa Yuda. Huu ndio uliokuwa upande wa magharibi.
15 Upande wa kusini mpaka ulianzia kwenye viunga vya Kiriath-Yearimu kwa upande wa magharibi, nao ukatokeza kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa. 16 Mpaka ukateremka hadi shefela inayotazamana na Bonde la Ben-Hinomu, kaskazini mwa Bonde la Warefai. Ukaendelea chini kwenye Bonde la Hinomu sambamba na mteremko wa kusini mwa mji mkubwa wa Wayebusi na kisha hadi En-Rogeli. 17 Kisha ukapinda kuelekea kaskazini, ukaenda hadi En-Shemeshi na kuendelea hadi Gelilothi, inayotazamana na Njia ya Adumimu, ukateremka hadi kwenye Jiwe la Bohani mwana wa Reubeni. 18 Ukaendelea upande wa mteremko wa kaskazini wa Beth-Araba ukateremka hadi Araba. 19 Kisha ukaenda mpaka kwenye mteremko wa kaskazini wa Beth-Hogla na kujitokeza kwenye ghuba ya kaskazini mwa Bahari ya Chumvi, kwenye maingilio ya Yordani upande wa kusini. Huo ulikuwa mpaka wa kusini.
20 Nayo Yordani ikawa ndio mpaka wa upande wa mashariki.
Hii ndiyo ilikuwa mipaka iliyoonesha urithi wa koo za Benyamini pande zote.
21 Kabila la Benyamini, kufuatana na koo zao, lilikuwa na miji ifuatayo:
Yeriko, Beth-Hogla, Emeki-Kesisi, 22 Beth-Araba, Semaraimu, Betheli, 23 Avimu, Para na Ofra, 24 Kefar-Amoni, Ofni, na Geba; miji kumi na mbili pamoja na vijiji vyake.
25 Gibeoni, Rama na Beerothi, 26 Mispa, Kefira, Moza, 27 Rekemu, Irpeeli, Tarala, 28 Zela, Elefu, mji wa Wayebusi (yaani Yerusalemu), Gibea na Kiriathi; miji kumi na nne, pamoja na vijiji vyake.
Huu ndio uliokuwa urithi wa Benyamini kwa ajili ya koo zake.