Zaburi 100
Dunia yote yaitwa kumsifu Mwenyezi Mungu
Zaburi ya shukrani.
1 Mpigieni Mwenyezi Mungu kelele za shangwe, dunia yote.
2 Mwabuduni Mwenyezi Mungu kwa furaha;
njooni mbele zake kwa nyimbo za shangwe.
3 Jueni kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mungu.
Yeye ndiye alituumba, sisi tu mali yake;
sisi tu watu wake,
kondoo wa malisho yake.
4 Ingieni malangoni mwake kwa shukrani
na katika nyua zake kwa kusifu,
mshukuruni yeye na kulisifu jina lake.
5 Kwa maana Mwenyezi Mungu ni mwema
na fadhili zake zadumu milele;
uaminifu wake unadumu kwa vizazi vyote.