Zaburi 112
Baraka za mwenye haki 
  1 Msifuni Mwenyezi Mungu.†kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.  
Heri mtu yule amchaye Mwenyezi Mungu,  
mtu yule apendezwaye sana na amri zake.   
 2 Watoto wake watakuwa wenye uwezo katika nchi,  
kizazi cha watu waadilifu kitabarikiwa.   
 3 Nyumbani mwake kuna mali na utajiri,  
haki yake hudumu milele.   
 4 Hata gizani nuru humzukia mtu mwadilifu,  
yule mwenye rehema, huruma na haki.   
 5 Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba,  
anayefanya mambo yake kwa haki.   
 6 Hakika hatatikisika kamwe,  
mtu mwenye haki atakumbukwa milele.   
 7 Hataogopa habari mbaya,  
moyo wake ni thabiti, ukimtegemea Mwenyezi Mungu.   
 8 Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu,  
mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake.   
 9 Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini;  
haki yake hudumu milele;  
pembe yake itatukuzwa kwa heshima.   
 10 Mtu mwovu ataona na kuchukizwa,  
atasaga meno yake na kutoweka,  
kutamani kwa mtu mwovu kutaishia patupu.   
*^ Zaburi hii imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
†Zaburi 112:1 kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.