Zaburi 113
Kumsifu Mwenyezi Mungu kwa wema wake
1 Msifuni Mwenyezi Mungu.*kwa Kiebrania ni Hallelu Yah; pia 113:9.
Enyi watumishi wa Mwenyezi Mungu msifuni,
lisifuni jina la Mwenyezi Mungu.
2 Jina la Mwenyezi Mungu na lisifiwe,
sasa na hata milele.
3 Kuanzia mawio ya jua hadi machweo yake,
jina la Mwenyezi Mungu linapaswa kusifiwa.
4 Mwenyezi Mungu ametukuka juu ya mataifa yote,
utukufu wake juu ya mbingu.
5 Ni nani aliye kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu,
Yule aliyeketi kwenye kiti cha enzi huko juu,
6 ambaye huinama atazame chini
aone mbingu na nchi?
7 Huwainua maskini kutoka mavumbini,
na kuwanyanyua wahitaji
kutoka lundo la majivu,
8 huwaketisha pamoja na wakuu,
pamoja na wakuu wa watu wake.
9 Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake,
akiwa mama watoto mwenye furaha.
Msifuni Mwenyezi Mungu.